RATIBA YA KILA SIKU YA KACHIKI
Kachiki
ni binti mdogo ambaye alikuwa anaishi kwenye kijiji cha Mwendapole. Kachiki
alikuwa akiishi na baba yake, pamoja na mama yake wa kambo aliyeitwa mama
Selina. Baba yake mzee Nyarongo na mama yake wa kambo walijaliwa kupata watoto
watatu, wanawake wawili na mvulana mmoja, Selina, Mwashamba na Malimo.
Kachiki
alikuwa ni binti mwenye akili sana darasani,
walimu wake walimpenda sana na hata pia wanafunzi wenzake. Lakini maisha
ya Kachiki nyumbani yalikuwa ni tofauti kabisa, yalikuwa ni maisha ya mateso ya
hali ya juu. Mama yake wa Kambo, mama Selina hakumpenda kabisa Kachiki. Alikuwa
akimtesa sana na kumpiga karibia kila siku wakati mwingine hata bila sababu ya
msingi. Alimwekea Kachiki ratiba ya kukusanya kuni na kuchota maji kila siku
kabla ya kwenda shule na akirudi shule pia.
Kachiki
hakuijua furaha wala amani, akiwa binti mdogo wa miaka 11 na akisoma darasa la nne
ndiye aliyekuwa mpishi mkuu wa pale nyumbani na mfanya kazi zote za pale
nyumbani. Ameanza kufanya kazi za pale nyumbani tangu akiwa darasa la kwanza na
akiwa na miaka nane tu. Kukusanya kuni, kuchota maji na kufua, kupika, usafi wa
pale nyumbani ndio zilikuwa kazi zake za kila siku. Pia alikuwa na ratiba ya
kwenda shambani kila ijumaa, jumamosi na jumapili. Matusi na vipigo navyo
vilikuwa ni sehemu ya maisha yake. Neno “furaha” na “amani” ilikuwa ni misamiati migumu sana kwake.
Watu
kwenye kijiji alichokuwa anaishi Kachiki walikuwa wanategemea maji kutoka mto
matumaini kwa matumizi yao ya kila siku. Mto ulipewa jina la matumaini
kwasababu ndiyo chanzo pekee cha maji
katika kijiji cha Mwendapole na ndiyo unaoleta matumaini kwenye familia nyingi hapo kijijini. Mto
matumaini upo mbali sana wanapoishi kina Kachiki. Inawachukua watu zaidi ya saa
moja kufika mtoni hapo. Mama yake wa kambo na Kachiki ameweka pipa ambalo Kachiki
anatakiwa kulijaza maji kila siku asubuhi kabla ya kwenda shule na jioni baada
ya kurudi shule. Na ili kujaza pipa hilo inambidi Kachiki arudie zaidi hata ya
mara nne na kila safari anabeba ndoo kichwani na kidumu mkononi.
Kachiki
amekuwa akichelewa shule karibia kila siku. Ratiba yake aliyopangiwa na mama
yake wa kambo mama Selina ni ngumu sana. Inabidi aamke saa 9 ya usiku kila siku
ili aweze kumaliza kazi zote alizopangiwa kabla ya kwenda shuleni.
Kila
siku Kachiki anaamka saa 9 ya usiku na kuchukua ndoo yake na kuelekea mtoni na
wasichana wengine wakubwa wa hapo
kijijini. Maana inabidi waongozane wengi kwa ajili ya usalama wao. Kila siku
asubuhi na jioni inabidi aende mtoni si chini ya mara tatu ili kujaza pipa
alilowekewa na mama yake wa kambo mama Selina.
Baada
ya pipa kujaa Kachiki anaenda kukusanya kuni zitakazotosha kwa ajili ya
matumizi ya siku hiyo. Baada ya kukusanya kuni anawasha moto na kuandaa chai ya
nyumba nzima. Siku zote Kachiki huanza kujiandaa kwenda shule kuanzia saa mbili
na nusu asubuhi na kuondoka saa tatu, wakati shuleni anatakiwa kufika saa mbili
asubuhi. Mara nyingi Kachiki amekuwa akichelewa sana kufika shuleni wakati mwingine
amekuwa akiwakuta wenzake tayari wapo mapumziko ya saa nne.
Mwanzoni
walimu wa Kachiki hawakuelewa kwanini Kachiki anachelewa sana kufika shuleni
hivyo alikuwa akiadhibiwa kila siku.
Kijiji cha kina Kachiki cha Mwendapole
USIKOSE KUSOMA HADITHI HII YA KACHIKI SEHEMU YA 2...