Translate

Tangazo la Hadithi

Wednesday, 26 June 2013

KACHIKI - SEHEMU YA 1


RATIBA YA KILA SIKU YA KACHIKI




Kachiki ni binti mdogo ambaye alikuwa anaishi kwenye kijiji cha Mwendapole. Kachiki alikuwa akiishi na baba yake, pamoja na mama yake wa kambo aliyeitwa mama Selina. Baba yake mzee Nyarongo na mama yake wa kambo walijaliwa kupata watoto watatu, wanawake wawili na mvulana mmoja, Selina, Mwashamba na Malimo.

Kachiki alikuwa ni binti mwenye akili sana darasani,  walimu wake walimpenda sana na hata pia wanafunzi wenzake. Lakini maisha ya Kachiki nyumbani yalikuwa ni tofauti kabisa, yalikuwa ni maisha ya mateso ya hali ya juu. Mama yake wa Kambo, mama Selina hakumpenda kabisa Kachiki. Alikuwa akimtesa sana na kumpiga karibia kila siku wakati mwingine hata bila sababu ya msingi. Alimwekea Kachiki ratiba ya kukusanya kuni na kuchota maji kila siku kabla ya kwenda shule na akirudi shule pia.

Kachiki hakuijua furaha wala amani, akiwa binti mdogo wa miaka 11 na akisoma darasa la nne ndiye aliyekuwa mpishi mkuu wa pale nyumbani na mfanya kazi zote za pale nyumbani. Ameanza kufanya kazi za pale nyumbani tangu akiwa darasa la kwanza na akiwa na miaka nane tu. Kukusanya kuni, kuchota maji na kufua, kupika, usafi wa pale nyumbani ndio zilikuwa kazi zake za kila siku. Pia alikuwa na ratiba ya kwenda shambani kila ijumaa, jumamosi na jumapili. Matusi na vipigo navyo vilikuwa ni sehemu ya maisha yake. Neno “furaha” na “amani”  ilikuwa ni misamiati migumu sana kwake.

Watu kwenye kijiji alichokuwa anaishi Kachiki walikuwa wanategemea maji kutoka mto matumaini kwa matumizi yao ya kila siku. Mto ulipewa jina la matumaini kwasababu ndiyo chanzo  pekee cha maji katika kijiji cha Mwendapole na ndiyo unaoleta matumaini  kwenye familia nyingi hapo kijijini. Mto matumaini upo mbali sana wanapoishi kina Kachiki. Inawachukua watu zaidi ya saa moja kufika mtoni hapo. Mama yake wa kambo na Kachiki ameweka pipa ambalo Kachiki anatakiwa kulijaza maji kila siku asubuhi kabla ya kwenda shule na jioni baada ya kurudi shule. Na ili kujaza pipa hilo inambidi Kachiki arudie zaidi hata ya mara nne na kila safari anabeba ndoo kichwani na kidumu mkononi.

Kachiki amekuwa akichelewa shule karibia kila siku. Ratiba yake aliyopangiwa na mama yake wa kambo mama Selina ni ngumu sana. Inabidi aamke saa 9 ya usiku kila siku ili aweze kumaliza kazi zote alizopangiwa kabla ya kwenda shuleni.

Kila siku Kachiki anaamka saa 9 ya usiku na kuchukua ndoo yake na kuelekea mtoni na wasichana wengine  wakubwa wa hapo kijijini. Maana inabidi waongozane wengi kwa ajili ya usalama wao. Kila siku asubuhi na jioni inabidi aende mtoni si chini ya mara tatu ili kujaza pipa alilowekewa na mama yake wa kambo mama Selina.
Baada ya pipa kujaa Kachiki anaenda kukusanya kuni zitakazotosha kwa ajili ya matumizi ya siku hiyo. Baada ya kukusanya kuni anawasha moto na kuandaa chai ya nyumba nzima. Siku zote Kachiki huanza kujiandaa kwenda shule kuanzia saa mbili na nusu asubuhi na kuondoka saa tatu, wakati shuleni anatakiwa kufika saa mbili asubuhi. Mara nyingi Kachiki amekuwa akichelewa sana kufika shuleni wakati mwingine amekuwa akiwakuta wenzake tayari wapo mapumziko ya saa nne.

Mwanzoni walimu wa Kachiki hawakuelewa kwanini Kachiki anachelewa sana kufika shuleni hivyo alikuwa akiadhibiwa kila siku.



Kijiji cha kina Kachiki cha Mwendapole




USIKOSE KUSOMA HADITHI HII YA KACHIKI SEHEMU YA 2...



No comments:

Post a Comment